Matokeo ya Darasa la Saba 2022 - 2023

  psle-2022 examination results - NECTA https://matokeo.necta.go.tz  › psle2022 › psle

Jumatano, 11 Aprili 2018

UHIFADHI WA FASIHI SIMULIZI


UHIFADHI WA FASIHI SIMULIZI

Ili kitu kidumu ni lazima kihifadhiwe; fasihi simulizi kama sanaa kutokana na umuhimu wake katika jamii nayo huhufadhiwa kwa ajili ya faida ya kizazi kijacho. Katika mada hii utaweza kujifunza umuhimu wa fasihi simulizi katika jamii. Utajifunza njia mbalimbali zitumikazo katika uhifadhi wa fasihi simulizi pia utaweza kubainisha ubora na udhaifu wa kila njia.
Umuhimu wa kazi za fasihi simulizi
Ingawa kila utanzu wa fasihi una umuhimu wake, kwa pamoja tanzu zake zote zina umuhimu mkubwa katika jamii.
v Fasihi hutumika kama chombo cha kuwaelimisha watu. Kupitia fasihi andishi na fasihi simulizi, watu hupata maarifa ya kutambua mambo maovu na namna ya kuyakwepa. Licha ya haya, wanajamii hujifunza njia za kujitawala, kuzalisha mali na kuishi kwa misingi ya haki, usawa na demokrasia.
v Fasihi ni nyenzo ya kutoa mafunzo kuhusu mambo kama vile historia, dini, siasa, jiografia na tiba. Kwa hiyo watu hujifahamisha juu ya maumbile na asili yake, mazingira, utawala, uchumi, sheria n.k. kwa kutumia fasihi simulizi au fasihi andishi.
v Fasihi huwapa watu mazoezi na kuimarisha uwezo wao wa kuzungumza kwa ufasaha, kuimba nyimbo kwa ufundi, kuigiza mambo kwa ustadi, kucheza ngoma kwa umahiri, kughani mashairi kwa mvuto na kusimulia matukio kwa mtindo ufaao.
v Fasihi hufahamisha, huhifadhi na hurithisha mambo kuhusu utamaduni kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Mambo hayo ni pamoja na mila, desturi, falsafa, imani na itikadi. Pia hudumisha maarifa ya kijadi kama vile tiba, sayansi ya kilimo, uhifadhi wa mazingira na sayansi ya utabiri wa hali ya hewa.
v Hutumika kama chombo cha kuburudisha na kupumbaza. Watu wanaposoma kazi mbalimbali za fasihi hupata, msisimko wa kimwili na kiakili. Kadhalika fasihi hugusa hisia za watu na kuwafanya wafurahi au wahuzunike.
v Fasihi hudumisha na kukuza lugha. Watu hupanua msamiati wao na miundo ya lugha kupitia kazi zake. Hivyo fasihi inakuwa kama hazina ya maneno na dafina ya kanuni za kisarufi.
Kutokana na umuhimu huu ndio maana fasihi huhifadhiwa ili isipotee. Na uhifadhi huu hufanyika kwa njia mabalimbali.

1.    Kichwani
Hii ndio njia ambayo imekuwa ikitumiwa kuhifadhi kazi za fasihi tangu kale na inaendelea kutumika hadi leo. Kwa kutumia njia hii kazi ya msanii hukaa kwenye ubongo wa msanii, naye huweza kuiwasilisha kazi hiyo, wakati wowote bila gharama yoyote.
Ubora wake
v Huweza kuwasilishwa muda wowote. uwasilishaji wa kazi hiyo unaweza kufanyika wakati wowote bila kuhitaji kufanyika maandalizi yoyote, hususani ya kiufundi.
v Hakuna gharama yoyote wakati wa uwasilishaji wa kazi ya fashi. Msanii hahitaji kugharimia kitu chochote ili waweze kuitoa kichwani, ni uamzi wake tu, anaweza kuimba papo kwa papo.
v Kazi ya fasihi iliyohifadhiwa kichwani ni hai. Hii ni kwa sababu msanii anakuwa ana kwa ana na hadhira yake. Kutokana na matumizi ya mbinu tofauti za kisanaa kama vile kucheza, kubadili sauti, miondoko na mengineyo mengi, kazi yake inapata uhalisia zaidi mbele ya hadhira.
Udhaifu wake
v Simulizi huweza kupotea kwa urahisi, kwa mtu aliyehifadhi kumbukumbu za akili zinaweza kupungua,au kufifia au fanani kufariki dunia. Hali hii ikitokea simulizi aliyoihifadhi katika ubongo/kichwa chake nayo hupotea.
v Huwa ni rahisi kubadili mambo muhimu katika simulizi hiyo. Hii inatokea pale ambapo msanii anasahau  baadhi ya maneno kutokana na umri wake au sababu nyinginezo.
v Kuna tatizo lakupata watu wanaoweza kuhifadhi kazi hizo kutokana na mazingira na mabadiliko yanayotokea katika jamii/ maisha.

2.   Njia ya maandishi
Kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia, fasihi simulizi inahifadhiwa katika maandishi kwaajili ya kumbukumbu za baadae. Njia hii imeanza kutumika baada ya watu kujua kusoma na kuandika. Uhifadhi wa kazi za fasihi kwa njia hii hupitia njia mbili kubwa.
*       Hatua ya kwanza ni kubuni kisa au wazo.
*       Hatua ya pili ni kuliweka wazo hilo katika maandishi.
 Kazi za fasihi simulizi zinazoweza kuhifadhiwa katika maandishi ni hadithi, nyimbo, mashairi, ngonjera, majigambo n.k
Ubora wake
v Hudumu kwa muda mrefu, Kazi iliyohifadhiwa katika maandishi inaweza kudumu kwa muda mrefu
v Huwafikia watu wengi zaidi, Kazi iliyohifadhiwa inaweza kufikia hadhira hata ya mbali na aliko msanii/ fanani.
v Fasihi simulizi ikihifadhiwa katika maandishi haipotezi fani na maudhui yake, Kazi iliyohifadhiwa katika maandshi haipotezi fani yake na maudhui yake bali huendelea kuwa katika asili yake ya awali hadi msanii atakapoamua kuibadilisha.
Udhaifu wake
v Njia hii hutumiwa na watu wachache hususani wale wanaojua kusoma na kuandika. Fanani na hadhira wanaoweza kutumia njia hii ni wale tu wanaojua kusoma na kuandika
v Ni gharama kubwa kuhifadhi fasihi simulizi katika maandishi. Msanii atalazimika kununua vifaa vinavyohitajika katika maandishi ambavyo ni kalamu, karatasi, meza, gharama za uchapaji n.k.
v Fasihi simulizi ikihifadhiwa katika maandishi hukosa uhai wake, Uwasilishaji wake si hai kwani hakuna kuonana ana kwa ana kati ya hadhira na fanani. Kwa hiyo msomaji hawezi pata vionjo vya msanii hivyo itambidi ajibunie yeye mwenyewe.
v Huwa ni mali ya msanii, fasihi simulizi ni mali ya jamii lakini ikishahifadhiwa katika maandishi inakuwa ni mali ya yule aliyeihifadhi kazi hiyo katika maandishi badala ya jamii nzima.
v Si kila kitu kinaweza kuhifadhiwa katika maandishi, maandishi kuna mambo ambayo kamwe hayawezi kuhifadhiwa katika maandishi. Mambo hayo ni yale yanayohusiana na utendaji ikiwemo sauti, vitendo, toni, kiimbo n.k.
v Haiwezi kubadilika kulingana na wakati na mazingira, hivyo hudumu katika hali yake ileile hata kama kuna makosa yaliyotendeka na msanii hayawezi kurekebishwa mpaka toleo jingine.

3.  Njia ya vinasasauti
Vinasasauti ni miongoni mwa vyombo vinavyotumika kuhifadhi kazi za fasihi simulizi. Hii ni njia iliyoendelea kuliko ile ya maandishi, vinasa sauti hushika sauti na vidoko vyake. Hivyo ili hadhira ipate kazi ya fasihi simulizi lazima anunue kanda hizo.
Ubora wake
v Kazi ya msanii huweza kuwafikia watu hata walio mbali na alipo mtunzi.
v Ikihifadhiwa katika vinasasauti kama vile tepurekoda au CD ubora wake huwa haupotei wala kuharibika endapo vifaa hivyo vitatunzwa vizuri.
v Sauti ya mtunzi unaiskia moja kwa moja
v Unaweza kusikia vionjo vya msanii
Udhaifu wake
v Kanda za kunasia sauti hushika sauti tu, hapa sauti huweza kusikika lakini matendo hayawezi kushikwa, kwa namna hiyo huweza kuathiri uhifadhi na utoaji wa kazi ya fasihi simulizi.
v Kukosekana kwa ushiriki wa hadhira, hapa sauti ya fanani husikika lakini haiwezekani kuonana ana kwa ana kati ya fanani na hadhira. Hivyo hadhira hushiriki kwa  kusikiliza sauti tu.
v Ni gharama kubwa kuhifadhi kazi ya fasihi simulizi kwa njia hii, kwanza huwa ni gharama kununulia kinasasauti pamoja na kununua kanda zenyewe, betri, n.k.
v Uwasilishaji wake si hai, ingawa unaweza sikia sauti ya msanii au wahusika lakini hawawezi kuonekana na hata hivyo haiwezi kubadilika kulingana na wakati na mazingira.
v Huwa ni mali ya msanii, Kazi yoyote ya kifasihi simulizi inapohifadhiwa katika vinasasauti, kwa mfano nyimbo, huwa ni mali ya msanii husika, mtu yeyote haruhusiwi kuitumia kama mali yake binafsi bila kuruhusiwa na msanii.

4.  Njia ya tarakilishi
Njia hii imeanza kutumika katika miaka ya hivi karibuni baada ya watu kuanza kujua na mna ya kutumia  kompyuta.
Ubora wake
v Njia hii ni ya uhakika zaidi kwa vile shuguli za kisanaa zinazohusika huhifadhiwa katika kompyuta na hutolewa pale zinapokuwa zinahitajika.
Udhaifu
v Msanii au wasanii wanohusika hawawasiliani na hadhira papo kwa papo. Hivyo hadhira hukosa kuuliza maswali katika vipengele vinavyotatiza.
v Hutumiwa na watu wachache, Ili kuhifadhi kazi ya fasihi kwa kutumia njia hii ni sharti msanii awe anajua kutumia kompyuta vilevile hadhira lazima ajue kutumia kompyuta.
v Njia hii ina gharama kubwa, ili uweze kuhifadhi fasihi simulizi kwa njia hii ni lazima uwe na kompyuta na ukizingatia kwamba kununua komputa ni gharama kubwa. Hivyo huwanufaisha tu wale wenye vyombo hivi vya kisasa.
v Njia hii inatumika zaidi mjini, ili kutumia kompyuta lazima mtumiaji awe na ujuzi na pia kuwepo na umeme hivyo wale wa vijijini na maeneo ambayo hakuna umeme hawawezi kupata kazi ya fasihi simulizi iliyohifadhiwa kwa njia hii.

5.    Njia ya kanda za video, televisheni na filamu za sinema.
Msanii huweza kutumia kanda ya video kuhifadhi kazi yake. Njia hii huweza kurekodi sura na sauti ya fanani. Hivyo kwa kutumia njia za filamu, za sinema na video tunawezakuhifadhi na kuonesha kazi za fasihi simulizi.
Ubora wake
v Kwanza wasanii na vifaa wanavyotumia huonekana,
v Sauti zao na milio ya ala wanazotumia husikika na pia huonekana kwa hadhira. Hii angalau huipa uhai kazi ya msanii mbele ya hadhira.
v Huweza kudumu kwa muda mrefu endapo kanda ya video iliyotumika kuhifadhi kazi ya msanii itatunzwa vizuri.
Udhaifu wake
v Uhifadhi wa njia hii unagharama sana, msanii atahitajika kununua, kanda ya video, kumlipa mpiga picha na mzalishaji pia.
v Watu wanoweza kunufaika na njia hii ni wacheche mno na wengi wao ni wale wenye uwezo wa kumiliki televisheni ambao kimsingi hupatikana maeneo ya mijini.
v Ingawaje hadhira wanaweza kumwona msanii lakini hawawezi kuwasiliana nae ana kwa ana, hivyo kukosa kuuliza swali pindi wanapohitaji kufanya hivyo.

Umuhimu wa kuhifadhi kazi za Fasihi Simulizi
v Ni muhimu kuzihifadhi kazi hizo zisiharibike wala kupotea ili ziendelee kutumika kutoka kizazi kimoja hadi kingine.
v Ni muhimu kuzihifadhi ili ziendelee kuwepo ili kuhifadhi utamaduni wetu na huku vikitumika kama vivutio kwa jamii na wageni/watalii.
v Kazi za fasihi simulizi kwa upande mwingine ni sehemu ya ajira. Kwa mfano, shughuli mabalimbali za kisanaa kama vile ngoma, maigizo na utunzi wa vitabu, vinawapatia vipato baadhi ya wasanii. Hivyo ni muhimu zihifadhiwe.
v Kazi za fasihi simulizi pia ni kichocheo cha umoja na maelewano miongoni mwa jamii.
Yote hayo kwa ujumla wake yanabainisha kuwepo na haja ya
kuendelea kuzikusanya, kuzifanyia kazi, kuziendeleza, na kuzihifadhi 
kazi za fasihi simulizi.

Jumapili, 1 Aprili 2018

Mtihani wa Kiswahili Kidato cha pili

WIZARA YA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI
SHULE YA SEKONDARI MWINUKO
 MTIHANI WA NUSU MHULA WA KWANZA MACHI 2018

KISWAHILI KIDATO CHA PILI.

Muda: SAA 2:00                                                                   Jumanne, 20 Machi 2018 mchana
Maelekezo
i. Karatasi hii ina sehemu A, B, C, D na E
ii. Jibu masali yote.
iii. Majibu yote yaandikwe kwenye nafasi ulizopewa.

SEHEMU A. (ALAMA 15)
UFAHAMU
i. Soma kwa makini habari ifuatayo kisha jibu maswali yanayofuata.
Kati ya lugha rasmi za jamii fulani moja inaweza kuteuliwa kuwa ni ya taifa. Kwa desturi, mbali na kutambuliwa kwa matumizi ya aina mbalimbali lugha ya taifa huwa ni kitambulisho cha taifa.
Mathalani kitu kinachomtambulisha Mngoni ni Kingoni chake. Hivyo basi kitambulisho cha kwanza cha mtu wa taifa fulani ni Lugha ya taifa hilo. Kwa jinsi hii, lugha ya taifa huakisi na kuchukua utamaduni wa taifa. Hivi ni kusema kwamba lugha ya taifa, hueleza ufasili wa taifa, kujenga umoja pamoja na kuwafanya watu wataifa hilo wajihisi kuwa wamoja.
Ingawa lugha rasmi inaweza kuwa lugha ya kigeni,haitokani na kundi lolote kati ya makundi yanayoikamilisha. Lakini lugha ya taifa mara nyingi huwa na mizizi ndani ya taifa lenyewe au huwa ni lugha inayozungumzwa na watu ndani ya nchi hiyo.
Kwa mfano ni muhali kisikia nchi moja ya Kiafrika kutangaza Kireno au Kiingereza kuwa lugha ya taifa. Linaloyamkinika hapa ni kuwa na mataifa yaliyotawaliwa na Wareno yatalazimika walau kwa miaka ya mwanzo kukitambua Kireno kuwa miongoni mwa lugha rasmi za taifa jipya.
Miongoni mwa sababu zinazofanya mataifa kuteua lugha ya asili kuwa lugha ya taifa lenyewe ni kwamba lugha hiyo haina budi kuwa inatumiwa na watu wengi na inaweza kufundishika kwa urahisi.
MASWALI
i. Pendekeza kichwa kifaacho kwa habari hii. ……………………………………………………
ii. Kwa mujibu wa habari hii lugha ya taifa hupatikanaje?………………………
iii. Bainisha sifa nne za lugha ya taifa
iv. Taja dhima tatu za lugha.
v. Nini maana ya maneno yaliyokolezwa wino kwa mujibu wa habari uliyoisoma?
a.      Kitambulisho ………………………………………………………………………
b.      Ufasili ……………………………………………………………………………….
c.      Muhali ……………………………………………………………………………...

SEHEMU B. (ALAMA 15)
MATUMIZI YA LUGHA NA USAHIHI WA MAANDISHI
2. A. Taja na fafanua kwa mifano mambo makuu manne ambayo mzungumzaji huzingatia katika kuteua maneno na miundo ya tungo zake. (alama 05)

   B. Onesha mazingira ambamo lugha ya tungo zifuatazo hutumika. (alama 05)
i.        Yesu anakupenda anataka akuokoe ………………………………………………….
ii.      Chapa hizi barua haraka haraka ……………………………………………………..
iii.    Nani chai ……………………………………………………………………………..
iv.    Kaza msuli baba, nyanyua zigo, twende juu………………………………………….
v.      Nipimie unga kilo tano………………………………………………………………..
C. Sahihisha makosa katika sentensi zifuatazo kwa kuziandika kwa usahihi. (alama 05)
i.                    Ninachukua nafasi hii kuwashukuru
Kosa: ……………………………………………………………………..
Sahihi: ……………………………………………………………………..
ii.                  Weka sahihi yako hapa.
Kosa: ……………………………………………………………………..
Sahihi: ……………………………………………………………………..
iii.                Sikuwa najua kuwa mwalimu wa Kiswahili anaitwa Mshiu.
Kosa: ……………………………………………………………………..
Sahihi: ……………………………………………………………………..
iv.                Katika ajali hiyo watu kumi waliuwawa.
Kosa: ……………………………………………………………………..
Sahihi: ……………………………………………………………………..
v.                  Ninakwenda kesho kwa mjomba.
Kosa: ……………………………………………………………………..
Sahihi: ……………………………………………………………………..

SEHEMU C. (ALAMA 15)
SARUFI
3. A.  Eleza waziwazi kuhusu kazi za viambishi vilivyopigiwa mstari katika maneno yafuatayo.  (alama 06)
(a)    A-nacheza (kazi mbili)
(b)    Ana-vi-penda (kazi mbili)
(c)    Ruk-a (kazi moja)
(d)  Ana-ye-fundisha (kazi moja) 
B. Kupitia taaluma ya unyambulishaji badili majina/Nomino zifuatazo-kuwa vielezi (alama 03)
i.        Nyumba ……………………………………………………………………............
ii.      Bustani …………………………………………………………………….............
iii.    Hewa ……………………………………………………………………................
iv.    Daraja ……………………………………………………………………...............
v.      Kitanda . …………………………………………………………………….............
vi.    Uwanja  ………………………………………………………………………………..
C.  Chunguza jedwali lifuatalo kwa makini kasha jaza sehemu zilizoachwa wazi. ( alama06)
Neno
Mzizi
Kauli ya Kutendana
Kauli ya Kutendwa
Kusema
………………
Kuomba
………………
……………….
……………. ……………. …………….
-andik-
…………….
…………………..
Kupigana
Kuombana
…………………..
Kuimbana
Kusemwa
…………………….
…………………….
Kuandikwa
……………. ………

SEHEMU D. (ALAMA 40)
FASIHI SIMULIZI
4. A. Kazi za fasihi simulizi zina umuhimu gani kwa jamii? (alama 10)
   B. Kamilisha methali zifuatazo. (alama 10)
i.        ………………………………………..…………… yasiyo na ncha.
ii.      Usidharau dafu …………………………….……………………….
iii.    …………………………………….…………si mwisho wa uhunzi.
iv.    ………………………………………………………… i maji.
v.      Mtumi wa kunga ……………………………..…………………
D. Eleza kwa ufupi maana ya dhana zifuatazo kwa kutumia mifano halisi. (alama 20)
        i. Ubeti
       ii. Kipande
       iii. Mizan
       iv.    Urari
        v.      Vina

SEHEMU E. ( ALAMA 15)
UANDISHI WA INSHA/UTUNGAJI
5. A. Mtumie simu ya maandishi baba yako aitwaye Michael Martin wa Sanduku la Posta 333 Moshi, ukiweleza kuhusu mdogo wako aitwaye Maringo Michael aliyevunjika mguu wakati akicheza mpira wa miguu katika mashindano ya UMISETA yaliyofanyika katika uwanja wa Shule ya Bwiru Wavulana. Jina lako ni Shukuru Michael. (simu yako iwe na maneno kumi tu )   (alama 05).

B. Chora kielelezo cha muundo wa Barua Rasmi. (alama 10)




------------------------------- MWISHO ------------------------------------
Jua na Mwezi Havifanyi Kazi kwa Pamoja Japo Vyote Hutoa Mwanga.
*******************************************************************************************
 † † † † †  MR. MSHIU S.E  † † † † †